Mazungumzo tete ya amani mjini Minsk kati ya viongozi wa Ukraine, Urusi, Ujerumani na Ufaransa yemendelea hadi leo, wakijadili mpango wa kukomesha mapigano ya miezi 10 nchini Ukraine. Mwanzoni mwa mazungumzo hayo marefu, rais wa Ukraine Petro Poroshenko alisisitiza juu ya usitishaji mapigano usiyo na masharti yoyote.
Chanzo kilicho karibu na mazungumzo hayo kilisema viongozi hao walipanga kusaini taarifa ya pamoja inayotoa mwito wa kutekelezwa kwa mpango wa amani wa awali uliyosainiwa kati ya serikali ya Kiev na waasi mwezi Septemba.
Jambo linalozua utata ni iwapo makubaliano mapya yatasogeza udhibiti wa waasi kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 500 waliloliteka katika kipindi cha mwezi uliyopita. Wanadiplomasia wa magharibi wameonya kuwa pande hizo zinaendelea kutofautiana kuhusu masuala muhimu, ikiwemo namna serikali ya Kiev inaweza kuimarisha ulinzi katika mpaka wake na Urusi wenye urefu wa kilomita 400, ambako inaituhumu Urusi kwa kupitishia silaha na wapiganaji. Msemaji wa rais Poroshenko amesema mazungumzo hayo huenda yakaendelea kwa zaidi ya masaa mengine matano hadi sita. Wakati huo huo, watu wasiopungua 49 wameuawa katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, wakiwemo 16 katika shambulizi baya la roketi mjini Kramatorsk, ambao ndiyo makao ya jeshi la serikali na kituo cha utawala mashariki mwa Ukraine.